Pages

Subscribe:

Thursday 29 January 2015

SIYO LAZIMA UANZE KUFANIKIWA WEWE, TIA MOYO WENGINE!




Ni wiki nyingine tunakutana kupitia safu hii ya Saikolojia, Maisha na Wewe. Natumaini kuwa umzima na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku kama kawaida.
Mimi namshukuru Mungu kwa kila jambo lakini kikubwa nimshukuru kwa kunifanya kuwa hivi nilivyo leo.
Ngugu zangu najua fika kwamba kila mtu anatamani mafanikio, kama wapo ambao wanaishi ili mradi siku zinakwenda ni wachache sana! Hii ni kwa sababu mafanikio ni kwa kila mtu.
Lakini pia ili ufanikiwe lazima uwe na subira, unaweza kupambana sana lakini ukashangaa mambo hayakunyookei. Hutakiwi kukata tamaa, kumbuka kufanikiwa hakuji kwa siku moja.
Hata hivyo, siyo lazima uanze kufanikiwa wewe, unapoona marafiki zako uliosoma nao, mliocheza pamoja enzi za utoto wenu au unaofanya nao kazi wamefanikiwa kabla yako, wala hutakiwi kuumia. Unatakiwa kuchukulia kwamba hiyo ni changamoto kwako na kupitia wao unaweza kufanikiwa.

Nasema hivyo kwa sababu wapo watu ni wa ajabu sana, yaani wakiona wenzao wamefanikiwa wanaumia sana na wakati mwingine kujenga chuki dhidi yao. Hiki ni kitu kibaya sana na ukweli mtu wa aina hiyo huwezi kufanikiwa.
Mwenzako anapofanikiwa wakati wewe bado mambo yanakuendea ndivyo sivyo, jenga ukaribu na mtu huyo na ikiwezekana pale ambapo unaweza kumshauri ili afanikiwe zaidi, fanya hivyo wala usiwe na kinyongo.
Unajua kwa nini? Kwa sababu kufanikiwa kwa rafiki yako ndiyo mwanzo wa kufanikiwa wewe. Akifanikiwa ndugu au rafiki yako na wewe ukawa na mchango kwenye mafanikio yake, ni wazi hata wewe utajipa imani kwamba unaweza kuwa kama yeye.
Pia huenda kwa kufanikiwa kwake akawa na mchango mkubwa katika safari yako ya kimafanikio kwani kama si kimawazo, kuna wakati hata kifedha anaweza kukusaidia ili na wewe utimize malengo yako.
 Yupo rafiki yangu ambaye ninapozungumzia suala la mafanikio, napenda kumtolea sana mfano. Huyu anaitwa Salum Kassim. Baba yake alikuwa na pesa sana na alipomaliza kidato cha nne, aliamua kufanya biashara akiamini ndiyo njia ya kumpatia mafanikio.
Nakumbuka kipindi kile aliniambia alikuwa na milioni 5. Akaanza kufanya biashara ya kununua mitumba Dar na kwenda kuuza Lushoto, Tanga. Kimsingi biashara ilimkataa lakini wakati huohuo alikuwa akifanya biashara na rafiki yake mwingine aitwaye Ford.
Ford alikuwa akifanya biashara sana hivyo Kassim akaona kwa kuwa yeye biashara imemshinda, ile pesa aliyokuwa nayo bora amuongezee mtaji Ford kisha yeye akasome.
Leo hii naambiwa Ford ana mafanikio makubwa sana na Kassim sasa anachukua shahada ya pili katika masuala ya sheria.
Mimi na wewe tunatakiwa kuwa kama Kassim, kijana ambaye aliona mafanikio yamemgomea lakini akaona kwa kuwa mwenza wake milango ya mafanikio imefunguka, bora ampe sapoti akiamini kama siyo leo basi kesho atanufaika na mafanikio yake.
Ndugu zangu kutiana moyo kwenye kutafuta mafaniko ni jambo la msingi sana. Hututakiwi kuwa na roho za kwa nini. Eti unaumia kwa sababu rafiki yako kafanikiwa, huo ni ulimbukeni.
Tushauriane, tutiane moyo pale inapobidi tukijua kabisa kwamba, kufanikiwa kwa mwenzako ni mwanzo wa wewe kufanikiwa.
Chanzo:gpl

0 comments:

Post a Comment