
Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Wabunge wa CCM, Anna Abdallah amesema wanachama wote wanaoendelea kukiuka kanuni na taratibu za chama hicho, lazima wachukuliwe hatua kali za kinidhamu.
Alisema chama kitapunguza heshima yake endapo
wanachama hao hawataadhibiwa kwa sababu walishapewa adhabu lakini
hawataki kujirekebisha.
Ingawa hakuwataja, waliopewa adhabu ni; Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wasira,
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja. Adhabu zao zinamalizika Februari
18, mwaka huu.
Kauli hiyo imekuja wakati Kamati ndogo ya maadili
ya chama hicho inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wake (Bara), Philip
Mangula, ikimaliza kazi ya kutathmini adhabu hizo juzi huku Katibu wa
Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye akisema inashangaza kuona baadhi
yao wakiendelea kufanya kampeni licha ya kamati Kuu ya CCM kupiga
marufuku.
Msimamo wa Anna Abdallah
Akizungumza jana, Abdallah ambaye ni Mwenyekiti wa
Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo), alisema chama hakitakiwi
kuogopa lolote juu ya kuwaadhibu wanachama hao.
“Mwanachama asipokuwa mtii wa kanuni za chama, huyo hatakiwi tena kuwa mwanachama, lazima ashughulikiwe na kama hataki kutii agizo la chama basi ajiondoe kwenye chama ili aende huko anakodhani kuna uhuru wa aina hiyo,” alisema na kuongeza:
“Chama kisiogope lolote kwani nidhamu inajengwa na
utii wa kutekeleza maagizo ya chama, kisipowachukulia hatua nadhani
inaweza kuleta athari kwa wengine kutotii maagizo.”
Kauli ya Nape
Akizungumza jana CCM Kisiwandui, Zanzibar baada ya
Kamati Ndogo ya Maadili kumaliza kazi ya kuwajadili viongozi wa
waliokumbwa na kashfa ya ufisadi wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow,
Nape alisema: “Chama hakitasita kuwanyima nafasi ya kuwania urais
wagombea watakaobainika na kudhibitika kuendelea kufanya kampeni kabla
ya wakati kinyume na mwongozo uliotolewa mwaka jana.”
Aliwataka wagombea na wapambe wao kuheshimu
utaratibu na uamuzi wa chama na wakati ukifika, kila mgombea atapewa
haki ya kufanya kampeni.
Alisema licha ya wagombea hao kutahadharishwa, lakini bado wapo na wapambe wao wanaondelea kufanya kampeni.
0 comments:
Post a Comment