Pages

Subscribe:

Wednesday 21 January 2015

Mapya yaibuka kuapishwa kwa mwenyekiti wa Segerea-Migombani


Wakili wa Kujitegeme, Iddi Msawanga(kulia) akimuapisha Japhet Kembo  (aliyenyanyua mkono) kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Migombani, katika hafla iliyofanyika nje ya ofisi za mwenyekiti wa mtaa huo,  Segerea Mwisho Dar es Salaam . Japhet aligombea nafasi hiyo kupitia chama cha Chadema

Siku moja baada ya wakazi wa Mtaa wa Segerea-Migombani jijini hapa kumwapisha mwenyekiti wao kwa kumtumia wakili wa kujitegemea, mapya yameibuka.
Uapishaji huo uliofanyika juzi nje ya ofisi za serikali ya mtaa huo, mbele ya umati wa watu na waandishi wa habari, umepingwa na ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa Manispaa ya Ilala iliyosema kuwa ni batili.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Segerea, Gango Kidera alisema jana kuwa wakazi wa mtaa huo wataendelea kupata huduma za kiserikali kutoka ofisi hiyo kama kawaida, kwa kuwa kitendo hicho kilizingatia sheria za nchi.
“Tunasubiri tuone mkurugenzi anataka kumweka nani badala ya kiongozi ambaye wananchi wamemchagua. Sababu za kutowaapisha viongozi waliochaguliwa hazijitoshelezi ndiyo maana wananchi wameshinikiza aapishwe na wakili wa kujitegemea na sheria zinaruhusu kwa kuwa zinataka mtu anayefanya hivyo ama awe hakimu au kamishna wa viapo,” alisema Kidera na kuongeza:
“Endapo kutakuwa na utata wowote utakaojitokeza baada ya mwenyekiti na wajumbe wake kuanza kutekeleza majukumu yao, basi nguvu ya umma itatumika kuamua hatma ya hali hiyo, tutaandamana na wananchi wanasubiri kuona hilo linatokea.”

Akizungumzia sababu zilizowasukuma kutafuta wakili badala ya kusubiri uchunguzi wa halmashauri, Kidera alisema kumbukumbu za ‘uchakachuaji’ wa matokeo ya uchaguzi mkuu uliopita bado hazijafutika.
Alipotafutwa Mbunge wa Jimbo la Segerea, Dk Makongoro Mahanga ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi na ajira ili aeleze kama anautambua uongozi uliosimikwa mtaani kwake, alidai kuwa kilichofanywa ni uvunjaji wa sheria za nchi, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa. Alisema mkurugenzi ndiye mwenye mamlaka ya kutangaza na kusimamia uchaguzi ikijumuisha pia kuapisha washindi kupitia wakili atakayemchagua na siyo vinginevyo, amewasihi Chadema kama waliweza kufuata utaratibu tangu mwanzo, ni vyema wakavuta subira kwa kumpa nafasi mkurugenzi ajiridhishe na uchunguzi wake anaoendelea kuufanya. “Siwezi kupanga kubadili matokeo. Wanaosema hivyo wana uoga,” alisema Dk Mahanga.
Ni woga tu ndiyo unaowasumbua kwasababu jina langu ni kubwa sana huku Segerea ndiyo maana wanaweweseka,” alisema Dk Mahanga.
Waziri huyo alisema kuwa haiwezekani kiongozi aapishwe barabarani na kama hilo linapata kibali mbele ya uongozi wa juu wa chama husika basi inewezekana tu kama wangefanya hivyo hata kabla ya uchaguzi kufanyika ili waeleweke kuwa ni wapindisha sheria, vinginevyo, wafuate utaratibu.

0 comments:

Post a Comment