Pages

Subscribe:

Wednesday 28 January 2015

SIMULIZI YA BINTI BIKIRA





Bado Latifa aliendelea kuwa kitandani hapo, ukimya ulikuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku, hakuwa akizungumza kitu chochote kile na hata kula alikuwa akila kwa kutumia mipira maalumu ambayo iliunganishwa tumboni mwake.
Kila siku ilikuwa ni huzuni kwao, kwa Bi Rachel, moyo wake ulikuwa kwenye maumivu makali mno, kila siku alikuwa akimuomba Mungu aweze kumponya binti huyo ili moyo wake urudi kwenye amani kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
Wiki zikakatika na hatimaye mwezi wa kwanza kumalizika, bado Latifa aliendelea kuwa kitandani pale. Mwezi mwingine ulipoingia, kidogo kwake ikaonekana kuwa nafuu, akaanza kwa kukunja vidole vya mikono yake, manesi waliokuwa ndani ya chumba hicho hawakutaka kubaki humo, wakatoka kwa kasi kumfuata Dk. Munil na kumwambia kile kilichokuwa kimeendelea chumbani.
“Kuna nini?” aliuliza Dk. Munil.
“Dokta, dokta, mgonjwa ameanza kukunja vidole vyake,” alisema nesi mmoja huku akihema kama mtu aliyekimbia umbali mrefu.
“Mgonjwa gani?”
“Latifa.”
Dk. Munil hakutaka kubaki ofisini kwake, kwa kasi ya ajabu akachomoka na kuanza kuelekea katika chumba alichokuwemo Latifa.
“Kuna nini?” aliuliza Bi Rachel ambaye alikuwa nje ya chumba kile.
“Subirini.”
“Kwa nini tusubiri? Manesi walitoka wakikimbia, wewe unatuambia tusubiri! Kuna nini?” aliuliza Bi Rachel huku Issa akiwa pembeni akimsikiliza.
Dk. Munil hakujibu swali hilo, akaingia ndani kwa ajili ya kujihakikishia kwa macho yake. Alipofika ndani ya chumba hicho, moja kwa moja macho yake yakatua kwa Latifa aliyekuwa kitandani, akayapeleka macho yake katika vidole vyake, kwa mbali vilikuwa vikitikisika.
“Amepona,” alijikuta akisema Dk. Munil huku akipiga magoti chini na kumshukuru Mungu.
Alichokifanya Dk. Munil ni kumuita Bi Rachel na Issa ndani ya ofisi yake na kuanza kuwaambia kile kilichokuwa kimetokea ambacho kwao kilionekana kama muujiza mkubwa.
Kila mmoja alijikuta akimshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyokuwa ameyafanya. Baada ya siku mbili, Latifa akaanza kufumbua macho yake na baada ya siku chache mbele, akaanza kuongea japo kwa sauti ya chini kabisa.
“Hakupata tatizo lolote?” aliuliza Bi Rachel.
“Hakupata. Tulitegemea angeweza kusahau kila kitu lakini haikuwa hivyo, tukahisi kwamba angeweza kupata ukichaa lakini haikuwa hivyo pia, ni mzima wa afya, hili ni jambo la kumshukuru Mungu,” alisema Dk. Munil.
“Kwa hiyo ni lini hali yake inaweza kutengemaa kabisa?”
“Hivi karibuni, nadhani baada ya wiki moja.”
“Tunashukuru sana.”
Waliendelea kusubiria hospitalini hapo huku kila mmoja akitaka kuona Latifa akirudi katika hali yake kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma. Kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele ndivyo ambavyo hali yake iliendelea kuwa vizuri na baada ya wiki moja iliyosemwa, akaanza kuongea kama kawaida.
“Ilikuwaje?”
“Ulipata ajali.”
“Mungu wangu!”
“Ila tunashukuru Mungu umepona.”
“Kwa hiyo hapa nipo hospitali gani? Agha Khan? Mbona Wahindi wengi?”
“Hapana. Hapa upo India.”
“Mmmh! Na wewe nani?” alimuuliza Bi Rachel.
Hakutaka kuficha, moyo wake ulikuwa ukimsuta kila alipotaka kukaa kimya. Hapo ndipo alipoamua kumwambia Latifa ukweli juu ya kila kitu kilichokuwa kimetokea. Moyo wa Bi Rachel ukaanza kumpenda Latifa. Katika maisha yake yote, alikuwa amepata mtoto mmoja tu ambaye kwa wakati huo alikuwa nchini Marekani akisoma. Jina la mtoto huyo aliitwa Godwin.
Mara baada ya kumzaa mtoto huyo, kwa bahati mbaya Bi Rachel akapata ajali mbaya ya gari akiwa na mume wake aliyefariki dunia palepale huku yeye akiharibika kizazi chake na kutokuweza kubeba mimba tena.
Akaishia kuwa na mtoto mmoja tu, hakupata mwingine tena, huyo ndiye mtoto aliyekuwa akimpenda. Kitendo cha kuwa karibu na Latifa kikamfanya kutamani kuendelea kuishi na msichana huyo, hakujua Latifa alikuwa nani, hakujua kama ana wazazi wake au la, kitu alichokuwa akikitaka ni kuishi naye tu.
“Nitamuomba niishi naye, nimsomeshe, nitatumia hata utajiri
wangu wote ili mradi afike pale ninapotaka afike. Halafu nilisikia wakisema kwamba yeye ni genius, kama ni kweli, nitampeleka Marekani katika shule ya watoto wenye vipaji akasome, nadhani huko maisha yake yatabadilika,” alijisema Bi Rachel, kila alipokuwa akimwangalia Latifa, alijisikia furaha moyoni mwake.
Chanzo:by2z.com

0 comments:

Post a Comment