Pages

Subscribe:

Monday 19 January 2015

‘Chuo kikuu ni fursa ya kuondoa ujinga, siyo kutafuta kazi’




Hivi karibuni nilialikwa kwenye makulaji ya kumaliza mwaka yaliyoandaliwa jijini hapa na Wafanyakazi wa Nice Catering Company yanye Makao Makuu yake Dar es Salaam.

Ilikuwa mara ya kwanza kuisikia kampuni hiyo, lakini nilipigwa na butwaa baada ya kupata taarifa kwamba ni kampuni kubwa ambayo ina wafanyakazi zaidi ya 700 wa kudumu katika maeneo mbalimbali nchini.
Risala ya wafanyakazi ilisema kampuni yao ina miaka 15 tangu kuanzishwa kwake na inatoa huduma za vyakula katika vikosi kadhaa vya jeshi, inamiliki hoteli, mabasi ya kusafirisha abiria na malori ya kubeba mafuta, vituo vya kuuza mafuta, maduka ya nguo katika majiji ya Arusha na Dar es Salaam.
Kwa kifupi ilielezwa kwamba ni kampuni inayoendeshwa na vijana wasomi wa kuanzia stashahada hadi shahada mbili na ina mameneja karibu 20.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Yona Sonelo akizungumza kwenye hafla hiyo alitoboa siri yake moja ambayo kwa kweli iliwaacha midomo wazi watu wengi.
Ni kweli mshangao uliwakumba waalikwa mbalimbali akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Mbeya ambaye alifika hapo kwa niaba ya mkuu wa mkoa aliyealikwa aje atoe zawadi kwa wafanyakazi bora wa kampuni hiyo.
Kauli ya Sonelo iliyowashtua wengi ilisema, “Kampuni yangu inaendeshwa na vijana wasomi wa kuanzia stashahada, shahada moja hadi mbili, lakini mimi nimemaliza vidato vitano tu,” alisema.
Sonelo anasema alianzisha kampuni Machi, 2000 kwa shida kubwa, lakini alizingatia kwamba polepole ndiyo mwendo. Anasema aliweka mkakati wa kuajiri vijana wenye ubunifu wa biashara ambao walioondoa ujinga wa kufikiria ajira baada ya kumaliza vyuo vikuu.
“Kwa hivyo moja ya sifa za walioajiriwa niliwauliza, baada ya kusoma walitarajia kufanya nini, waliotoa mipango ya kazi ndiyo niliowaajiri, lakini waliosema wanatafuta kazi zikuwataka,” anasema.
Anasema hadi sasa ana msimamo huo kwa sababu anatambua wazi kwamba kusoma kwenye vyuo vikuu ni fursa ya kuondoa kabisa ujinga na siyo fursa ya kuanza kutafuta kazi.
“Kwanza nina uhakika vijana wanaomaliza vyuo kila mwaka ni wengi mno, wanafikia hata 100,000. Je, ni kweli wote wanaweza kupata kazi Serikalini,’’ alihoji.
Anasema hata ije Serikali ya aina gani, kamwe haiwezi kutatua tatizo la ajira kwa vijana wote wanaomaliza vyuo vikuu bali kinachotakiwa ni kwa wahitimu wenyewe kukaa chini na kubuni kazi za kufanya.
“Jamani tusishangae vijana kukosa ajira Tanzania, hata nchi jirani ya Kenya wapo vijana wenye shahada wanaouza mitumba na huko Nigeria wapo wenye shahada wanaofanya kazi ya kufagia barabarani.
“Lakini pia wapo vijana waliobuni miradi na hatimaye kusaidiwa na Serikali katika kufanikisha malengo,” anasema.
Sonelo anaishauri Serikali kwamba pamoja na mazingira mazuri ya uwekezaji, itoe kipaumbele ya kuwasaidia kwa fedha wahitimu nchini waweze kuwekeza kwenye miradi waliyoibuni ili watoe ajira kwa vijana wenzao.
Hoja hiyo inafafanuliwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Dk Norman Sigalla anasema ni kweli Serikali ina wajibu wa kuhakikisha mazingira mazuri ya uwekezaji yanatolewa kwa Watanzania.
Dk Sigalla akitoa angalizo anasema, asilimia 60 ya matajiri duniani ni wale ambao hawakufika hata chuo kikuu.
Anasema wafanyabiashara wengi waliofanikiwa ni wale wasio na shahada na shahada za uzamili au uzamivu na kwamba wengi ni watu wa kawaida.
“Maendeleo ya mtu yanatokana na mtu mwenyewe kujua kutafisiri kwa usahihi matatizo ya jamii na hatimaye kutafuta ufumbuzi,” anasema na kuongeza kwamba tatizo la wahitimu wengi wa vyuo vikuu wa sasa bado wana imani za kizamani kutaka kuwatumikia watu wengine.
“Enzi za Mwalimu, wasomi walikuwa wachache na
ndiyo maana hata mtumishi akifanya madudu hapa alipata uhamisho kwenda kwingine, lakini sasa hivi nafasi zimejaa kila mahali, hivyo wahitimu wa vyuo vikuu wawe na mtazamo wa kijiajiri na kuajiri wengine,” anasema.

0 comments:

Post a Comment