
HABARI zenu wapendwa wasomaji wa safu hii. Nimefurahi tumekutana tena kwa mara nyingine ili kupeana mawili matatu yanayohusu mahaba,
Juzi nilikuwa na rafiki yangu mmoja tumekaa sehemu tunabadilishana mawazo, akanipa simulizi ambayo imezaa mada hii. Alinisimulia mkasa wake kuwa anahisi mke wake anatoka na mtu mwingine, kwa sababu baada ya kuishika simu yake kwa siri na kuipekua, alikutana na baadhi ya sms zilizompa utatanishi kidogo, ingawa alishindwa kujiridhisha moja kwa moja kuwa zilikuwa zinatoka kwa mwanaume.
Baada ya kukutana na tukio hilo, kwa sababu alishindwa kumuuliza mkewe
kwa hofu ya kuonekana kupekuapekua simu yake, basi alichofanya ni
kumkumbuka mmoja wa michepuko yake kisha akapanga naye kukutana sehemu
ili kuondoa stress.
Hapo ndipo nilipojikuta nabaki hoi, kwani aliniambia kila mara
inapotokea hali kama hiyo, anachofanya ni kutoka nje ya ndoa yake na
akishafanya hivyo, roho yake hubaki kwatu. Sababu kubwa ya kufanya
hivyo, kwa mujibu wa maelezo yake, eti kama mbwai na iwe mbwai tu.
Ingawa nilimsikiliza na kumwelewa, lakini sikutaka kumuacha aendelee
kuwa na tabia hiyo, siyo kwa uwezekano wa magonjwa ya zinaa, bali
kisaikolojia, akili yake anaiweka katika sehemu ambayo haimsaidii.
Dawa ya kupigwa ngumi haiwezi kuwa kurudisha ngumi kwa sababu ugomvi
hautakwisha. Ili kuondoa ngumi, ni lazima kukaa na anayekupiga ili kujua
sababu ya kukupiga, maana huenda unafanya kosa bila wewe kujua kama
unakosea.
Unajaribu kujiuliza, kama mke atapata hisia za kusalitiwa na mume wake,
halafu na yeye akatoka nje ili kulipa kisasi, hii itakuwa ni ndoa ya
aina gani? Yaani watu hao wawili wakihisiana tu, ndani kumechafuka,
kila mmoja anatoka kumtafuta mbadala!

Kama tunaamini katika mapenzi au ndoa zetu, basi dawa nzuri ya kuhimili
kutendwa, ni kukaa na mwenza wako na kumueleza kwa uwazi kuhusu hisia
zako, kwani hilo ndilo suluhisho la kudumu na tena lililo salama.
Mwambie kuhusu ujumbe mfupi wa maneno ulioukuta katika simu yake, huenda anaweza kukuondolea hofu yako kwa kutoa ufafanuzi ambao utauelewa.
Mwambie kuhusu ujumbe mfupi wa maneno ulioukuta katika simu yake, huenda anaweza kukuondolea hofu yako kwa kutoa ufafanuzi ambao utauelewa.
Watu wengi walio katika uhusiano au ndoa, hutikisa uhusiano wao kwa
sababu ya hisia tu pasipo ukweli wowote. Ni kwa sababu tu amesikia
akiongea na sauti ya kike au ya kiume, basi moja kwa moja huamua kuamini
kuwa anayezungumza naye ni mpenzi wake.
Nimeshawahi kusema huko nyuma, kwamba hakuna raha katika uhusiano wa
kimapenzi kama kujifanya kama vile humuoni mwenza wako na wala
humfuatilii. Unampenda, lakini usiruhusu akili yako iumie juu yake.
Achana na simu yake, mwache azungumze kadiri anavyotaka na wala usihoji
kuhusu mwanamke au mwanaume uliyemuona naye.
Anayesaliti hujitambulisha mwenyewe, kama ni simu, ataenda kuongelea
mbali na wewe ulipo, kama ni ujumbe wa simu, basi atakutazama kwanza
kabla ya kujibu na vitu vingine kama hivi. Unapomtambua kwa dalili hizi,
unamuumiza zaidi kama hutamuuliza kwa sababu hataelewa unachokiwaza
moyoni mwako!
0 comments:
Post a Comment