Pages

Subscribe:

Wednesday 21 January 2015

Kauli ya Mwakyembe yaamsha wadau


Shirika la Ndege la Flight Link la Dar es Salaam limesema litaanza kutoa huduma ya usafiri wa anga kati ya Dar es Salaam na Iringa muda wowote kuanzia sasa.
Uamuzi wa Flight Link kuanzisha huduma hiyo, umekuja siku chache baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kufanya ziara mkoani hapa na kushawishi wadau wa usafiri wa anga kutoa huduma mkoani hapo.
Mwakyembe alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akiwa kwenye ziara mkoani Iringa na kupokea taarifa kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Thomas Haule ambaye alisema kumekuwa na ongezeko kubwa la abiria wanaotumia usafiri wa anga.
Ripoti ya TAA ilionyesha kuwa mwaka 2009, idadi ya abiria ilikuwa 756, lakini kufikia mwaka 2013, idadi hiyo sasa imefika 9,808.
Mkurugenzi wa Masoko wa Flight Link, Ibrahim Bukenya alisema wana mpango wa kutoa huduma mara tano kwa wiki kati ya Uwanja wa Ndege wa Nduli na Dar es Salaam.
Alisema kuwa ndege wanayotarajia kuitumia kusafirisha abiria ina uwezo wa kubeba abiria 30.
“Ndege itakuwa ikiondoka Iringa asubuhi kupitia Dodoma hadi Dar es Salaam,” alisema Bukenya na kuongeza:
“...Kutegemeana na idadi ya abiria jijini hapa, lakini lengo letu ni kutoa huduma Jumatatu, Jumanne, Jumatano, Alhamisi na Ijumaa.”
Alisema usafiri huo utawasaidia wananchi, wakiwamo wafanyabiashara kutumia muda mfupi kusafiri kutoka eneo moja hadi jingine, hivyo kuongeza ufanisi.
Flight Link wanakuwa wadau wa pili wa usafiri wa anga kutoa huduma kati ya Iringa na Dar es Salaam.

Shirikla la Auric Air ndilo ambalo ndilo linalotoa huduma hiyo kwa sasa.

0 comments:

Post a Comment