Ni
matumaini yangu kwamba una shauku kubwa ya kujua nini nimekuandalia kwa
leo. Ni yaleyale kuhusu maisha yetu ya kimapenzi na leo nataka
kuzungumzia usaliti katika sura ya tofauti.Nimefikia uamuzi wa kuandika
juu ya hili kutokana na ushuhuda nilioupata kutoka kwa mmoja wa wasomaji
wangu aliyejitambulisha kwa jina la Ashura mkazi wa Arusha.
Ni ushuhuda wa kusikitisha sana lakini una funzo ndani yake kwa wanandoa na wapenzi wa kawaida.
Anasemaje? Hebu msikie kwanza kisha tuendelee; “Mimi na mume wangu
tulikuwa tunapendana sana na hajawahi kunisaliti. Tulioana miaka mitatu
iliyopita na sasa nina ujauzito wa miezi nane.
“Mume wangu anafanya kazi na mimi pia nafanya kazi lakini kipato changu ni kikubwa kumzidi mume wangu.
“Kutokana na hali hiyo, mimi nilinunua gari ambalo mume wangu amekuwa
akilitumia muda mwingi. Huwa ananipeleka kazini kisha yeye anaenda
kwenye mihangaiko yake, jioni ananifuata. “Tunaishi na mdogo wangu wa
kike ambaye anasoma chuo ila alionesha ukaribu sana kwa mume wangu,
utani ulikuwa mwingi hadi kuna kipindi nikahisi kuna kitu nyuma ya
pazia.
“Siku moja baada ya mume wangu kunipeleka kazini, tulimuacha nyumbani
yule mdogo wangu, ilikuwa aende chuo lakini nikashangaa siku hiyo
akasema hataenda. “Machale yakanicheza! Baada ya mume wangu kunifikisha
kazini na kuondoka, nikakaa kama nusu saa hivi kisha nikachukua Bajaj na
kurudi nyumbani.
“Huwezi kuamini nilimkuta mdogo wangu akifanya mapenzi na mume wangu
juu ya kitanda changu. Nilipata presha na kuanguka, nilipozinduka
nilijikuta nikiwa hospitalini.“Mpaka sasa niko kwa wazazi wangu na
nakaribia kujifungua. Hivi kwa usaliti huu naweza kumsamehe mume wangu
na tukaishi kwa amani?”
Huo ni ushuhuda wa Ashura ambaye mwisho wa
siku aliomba nimshauri. Ingekuwa wewe ungemshaurije? Je, ungemshauri
arudi kwa mumewe au ungemtaka aombe talaka?
Najua kwa vyovyote ungekuwa na la kumshauri lakini mimi ninavyoona
kwa hili ni lazima uwe njia panda. Yaani mdogo wako umkute kamvulia nguo
mumeo na wanafanya uzinzi juu ya kitanda chako! Ukisikia watu wanaua ni
katika mazingira haya.
Hata
hivyo, kabla sijamshauri Ashura nikuulize wewe msomaji wangu, je, upo
usaliti ambao unaweza kusema huu unavumilika na huu hauvumiliki?
Kimsingi watu tunatofautiana jinsi tunavyopokea yale yanayotupata.
Wapo ambao wamewafumania wanandoa wenzao mara kibao lakini mpaka leo
bado wanaishi pamoja na wanasimamia ule msemo usemao; ‘Yaliyopita si
ndwele, tugange yajayo’.Lakini wakati hao wakiwa na mioyo hiyo, kuna
ambao wameachana baada ya mmoja kukuta tu sms tata kwenye simu ya mwenza
wake.
Kwa hili la Ashura iko hivi, hakuna usaliti usiouma, uwe ni mdogo au
mkubwa. Usaliti aliofanyiwa Ashura ni mkubwa sana, huwezi kumshauri
kirahisi tu kwamba amsamehe mume wake na arudi kwake.Lakini pia huwezi
kumshauri kwamba kwa kuwa ni usaliti mkubwa basi asimsamehe na aombe
talaka.
Ushauri wote unaweza kuwa sawa lakini pia unaweza usiwe sawa.
Kutokana na mazingira, kwamba Ashura ni mjamzito na mume wake hajawahi
kumsaliti, kuna kila sababu ya kusamehe.Kama mume ameomba msamaha na
kuahidi kubadilika, kumgomea itakuwa ni vigumu.
Lakini naomba niseme kwamba, kwenye suala la usaliti ni vyema
tukazungumza na mioyo yetu. Ukijaribu kufuatilia utabaini hakuna ambaye
hajawahi kusalitiwa na mpenzi wake. Tunachokifanya huwa ni kusamehe na
kusahau hasa tukichukulia kwamba, wote tuna mapungufu. Ni kweli kuna
usaliti usiovumilika, kwa mfano kama amekuwa akikusaliti kila wakati,
huyo ifike wakati useme imetosha.
Lakini kama unampenda na kwa bahati mbaya akawa amekusaliti kwa mara
ya kwanza, ni vyema ukampa nafasi nyingine bila kujali watu watasemaje.
Kwa maana hiyo licha ya kwamba usaliti si mzuri lakini usichukue uamuzi
wa kumuacha mwenza wako au mpenzi wako kwa sababu ya usaliti wa mara ya
kwanza, ukifanya hivyo ipo siku utajuta.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments:
Post a Comment