Pages

Subscribe:

Monday 21 July 2014

Mikato ya nywele ya ajabu Kombe la Dunia 2014





Kombe la dunia ni tukio kubwa zaidi la soka duniani. Fainali za Kombe la 2014 ambazo zilianza Juni 12 tayari zimemalizika Julai 13 wiki iliyopita huku timu ya Ujerumani ikitawazwa kuwa mabingwa wapya wa soka duniani.
Kulikuwa na timu 32 zilizoshiriki na kila mchezaji aliyeshiriki alijaribu kwa njia yake ya kupata umaarufu katika tukio hili muhimu katika historia ya soka.
Ukiachilia mbali uchezaji wao, baadhi ya wachezaji walitumia mitindo ya nywele zao kupata umaarufu katika tukio hilo muhimu. Walikuja na mikato na mitindo ya kipekee inayoweza kutumika kama utambulisho wao.
Katika mitindo hiyo ya nywele ilikuwapo ile ya kuvutia unayoweza kuitumia na bado ukaonekana nadhifu, lakini pia ipo ile mingine iliyowafanya wahusika waonakane wa ajabu kuwa kwenye mitindo ya kituko.
Je, unapenda kujua ni nyota gani walikuwa katika mitindo ya ajabu kwenye Fainali za Kombe la Dunia kule Brazil?, wafuatao ni nyota hao:
Rodrigo Palacio: Argentina
Mfungaji wa timu ya Argentina, Rodrigo Palacio aliyekuwa miongoni mwa wachezaji walioipeleka timu yao kwenye fainali za kombe hilo, anashika nambari moja kwenye wachezaji walioko kwenye kundi hili. Akiwa kwenye mtindo wake wa nywele unaofanana na mkia wa panya, alinyoa nywele zake zote na kubakisha kisogoni tu, aliposuka butu moja na kulining’iniza. Licha ya kuoenekana kama kituko, lakini mtindo wake ulionekana kuwavutia wengi.
Raul Meireles: Ureno
Akiwa timu moja na Cristiano Ronaldo, muonekaao wa Raul Meireles katika fainali hizi ulimfanya apate umaarufu kirahisi kwa watazamaji wa kombe la dunia.
Alikuwa katika mtindo wa kiduku, lakini tofauti na ule wa mchezaji wa timu ya Italia, Mario Balotelli, yeye alikwangua upara na kuacha katikati nywele zilizochachamaa mithili ya upanga wa jongoo.
Bacary Sagna: Ufaransa
Beki wa kulia wa timu ya Ufaransa, Bacary Sagna naye alijipatia umaarufu kutokana na muonekano alioingia nao. Alisuka nywele zake kwa kutumia rasta za rangi nyeupe na hivyo kubadilisha kabisa muonekano wake. Unapotaja mitindo ya ajabu ya nywele kuwahi kutumiwa na wachezaji wa mpira wa miguu kwenye kombe la dunia, huwezi kuweka pembeni mtindo wa nyota huyu.
Kyle Beckerman: Marekani
Kiungo wa timu ya Marekani, Kyle Beckerman huyu naye alikuja na mtindo wake wa rasta. Tofauti na zile za Bob Marley, rasta za Kyle zilikuwa zinaonekana kama zimechoka hivi, unaweza kudhani kuwa hazijafanyiwa marekebisho muda mrefu. Kwa kifupi zilionekana kama msitu hivi. Jambo hili lilichangia aonekane wa kipekee na wa ajabu ajabu vile vile. Kwa upande mwingine mtindo wake huu wa nywele ulichangia kutoa utambulisho wake na hivyo kupata umaarufu pia.

Paul Pogba, Ufaransa
Mchezaji wa timu ya Ufaransa aliyekuja na mtindo wake wa nywele. Kwa mbali mtindo huu unafanana na kile kiduku cha Mario Balotelli, lakini yeye ameongeza mbwembwe na kuweka mistari kwa pembeni. Mistaru hiyo imewekwa kwa kutumia ‘bleach’ hivyo kuonekana kwa urahisi kama unavyomuona hapo pichani.
Geoffrey Serey Die: Ivory Coast
Mtindo mwingine wa ajabu wa nywele katika Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2014, ni ule wa mchezaji wa kati wa timu ya taifa ya Ivory Coast Geoffrey Serey Die. Kama ilivyo kwa Pogba, nyota huyu naye amekuja na mtindo wa kiduku cheupe. Kama anavyoonekana hapo pichani, amenyoa nywele zake kwa ngazi, ambapo katikati ameziacha na kuzipaka bleach.

0 comments:

Post a Comment