Pages

Subscribe:

Wednesday 16 July 2014

Mbrazil mpya wa Yanga... mambo mazito




YANGA noma! Ndivyo unavyoweza kusema kwa sasa baada ya jana kutimiza idadi ya Wabrazili wanne watakaoitumikia klabu hiyo msimu ujao kwa kumleta nchini mshambuliaji mpya kutoka nchini humo, Genilson Santana Santos ‘Jaja’.
Genilson Santana Santos ‘Jaja’ alipowasili nchini.
Jaja ambaye ametua nchini jana majira ya saa 8.30 mchana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) Dar, anatarajiwa kuwa mrithi wa Emmanuel Okwi raia wa Uganda anayetarajiwa kufungashiwa virago kutokana na kuvurugana na uongozi wa klabu hiyo, lakini kutua kwake kulizua zogo kubwa kutokana na ragi ya tisheti yake.
Kutokana na ujio wa Jaja anayesifika kwa kucheka na nyavu na kupiga mashuti ya mbali, sasa Yanga imetimiza idadi ya Wabrazili wanne, wengine ni kocha mkuu, Marcio Maximo, msaidizi wake, Leonardo Neiva na kiungo mshambuliaji, Andrey Coutinho.
Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Jaja alipokewa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mohammed Binda na ofisa habari wa timu hiyo, Baraka Kizuguto, aliyesema kuwa mshambuliaji huyo hawezi kuongea neno lolote kwa mashabiki waliojitokeza kumlaki kutokana na kutojua kuongea Kiingereza, zaidi ya Kireno pekee.

.....akisaini.
Baada ya hapo, Jaja alipiga picha na mashabiki hao kisha kuanza safari ya kuelekea kwenye Makao Makuu ya Yanga yaliyopo Jangwani, Kariakoo jijini Dar kwa ajili ya utambulisho rasmi.
Msafara huo uliokuwa na nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki hao, ulikuwa na magari manne waliyopanda na moja alilokuwemo Jaja.
Kejeli za mashabiki wa Simba zilizomkumba Maximo siku aliyotua nchini wakati anakatiza Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo kwenye makao makuu ya wapinzani wao hao, ndizo zilizomkuta Jaja baada ya kuambiwa kuwa, ametua nchini kuwaletea Yanga majanga ya kufungwa mabao 7-1 kama ilivyotokea juzi kwenye Kombe la Dunia, Brazil ilipopigwa bao hizo na Ujerumani kwenye mchezo wa nusu fainali.
Haikuishia hapo, kwani msafara huo ulizomewa kwa maneno mbalimbali ya ‘shombo’ huku Wanasimba hao wakionyesha alama ya vidole vitano wakimaanisha mabao 5-0 waliyoifunga timu hiyo misimu miwili iliyopita.
Hatimaye wakawasili makao makuu ambapo huko nako mashabiki waliokuwa wakiwangojea, walilipuka kwa furaha na kuanza kuliimba jina la Jaja wakati anashuka na kumsalimia kwa kumshika mkono na moja kwa moja akaelekea kwenye ofisi za klabu hiyo na kusaini katika kitabu cha wageni.
Genilson Santana Santos ‘Jaja’akiwapungia mkono mashabiki wa Yanga.
Baada ya hapo, alipanda juu ya jengo la klabu hiyo kwa ajili ya kwenda kutambulishwa kwa mashabiki ambapo kwa mara ya kwanza Jaja akaongea Kiswahili kwa kutamka ‘Yanga oyee’ na kuitikiwa kwa shangwe na mashabiki hao.
Lakini baada ya hapo, mashabiki hao wakaanza kulaumu tena kwa nini hakuvishwa jezi ya Yanga na kumuachia avae fulana ya rangi ya pink aliyokuja nayo ambayo baadhi yao walisema ni rangi nyekundu inayowakilisha Simba hali ambayo ilizua zogo upya, jambo ambalo lilimfanya Binda alitolee ufafanuzi.
Binda alisema: “Sisi wenyewe tulitaka kumpa jezi yetu lakini katibu mkuu, Njovu (Benno) hayupo na yeye ndiye mwenye funguo za ofisi ambayo ina jezi, kwa hiyo kwa taratibu za kiofisi haturuhusiwi kwenda kufanya hivyo.”
Baada ya maneno hayo, mashabiki walionekana kuridhika na ufafanuzi huo, kisha taratibu nyingine zikafuata ambapo Binda aliongeza: “Haya ndiyo yale majibu ya ahadi ya mwenyekiti (Yusuf Manji) kwamba alisema ataifanya Yanga iwe ya kimataifa kwa kuanza na benchi la ufundi na sasa amegeukia kwa wachezaji.”

0 comments:

Post a Comment